Monday, July 13, 2015

Dk Magufuli Achaguliwa kugombea urais kwa tiketi ya CCM


CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimempitisha Dk. John Pombe Magufuli kuwa mgombea urais kupitia chama hicho. Anandika Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).
Katika Mkutano Mkuu uliofanyika usiku wa kuamkia leo mjini Dodoma, Dk. Magufuli amechaguliwa kwa kura 2104 sawa na asilimia 87.08, akifuatiwa na Balozi Amina Salum Ali aliyepata kura 253 sawa na asilimia 10.4 na Asha-Rose Migiro aliyepata kura 59 sawa na asilimia 2.44702.


Jumla ya kura zilizopigwa kwenye Mkutano Mkuu wa CCM kumchagua Mgombea atakayepeperusha bendera ya CCM kwenye uchaguzi Mkuu wa 2015 ni kura 2422, kura zilizoharibika ni sita, kura halali walizopigiwa wagombea ni 2416.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya kikao hicho, Dk. Magufuli amepita kwa kura hizo kutokana na nguvu yake dhidi ya wagombea wengine.
“Hakukuwa na namna hapa kwa kuwa, wajumbe wanaamini katika mazingira haya magumu ya upinzani Dk. Magufuli anaaminika na kukubalika nje kuliko hawa wengine,” anasema mtoa taarifa na kuongeza;
“Baada ya kutemwa Membe (Bernard Membe) kwenye NEC kila mjumbe ambaye alikuwa upande wa Lowassa (Edward Lowassa) alipumua jambo lililomrahisishia Magufuli.”
Mkutano huo umehairishwa mpaka saa nne asubuhi, ambapo ndiyo muda ambao Dk. Magufuli ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Biharamulo Mashariki na Waziri wa Ujenzi atatangazwa rasmi kuwa mgombea wa Urais kupitia chama hicho.
Awali ndani ya ukumbi wa mkutano, kulidawa kuwepo kwa mpango wa wafuasi wa Lowassa kutaka kumpitisha Balozi Amina ili chama hicho kipate changamoto katika ‘kumuuza’ kwa wananchi ikiwa ni kulipiza kisasi kwa kukatwa mtu wao (Lowassa).
Katika Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya chama hicho, majina yaliyopitishwa yalikiwa ni Migiro, Magufuli, Balozi Amina, Membe na January Makamba.
Katika Halmashauri Kuu ya CCM yalipita majina matatu ya Dk. Magufuli, Dk. Migiro na Balozi Amina.